Uchunguzi wa Dosari za Kimofosintaksia Zinazofanywa na Wajifunzaji wa Kiswahili katika Shule za Upili Nchini Uganda

Authors

  • Anifa Atuhaire Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Abstract

Makala haya yanawasilisha matokeo ya utafiti kuhusu dosari za kimofosintaksia zinazofanywa na wajifunzaji wa Kiswahili katika shule za upili nchini Uganda. Data iliyochunguzwa katika makala haya ni sehemu ya data iliyokusanywa uwandani kati ya mwezi Februari na Machi 2023 kwa ajili ya tasnifu ya uzamivu. Data hiyo ilikusanywa katika eneo la Ankole katika wilaya za Mbarara, Bushenyi na Ibanda. Sampuli ilihusisha shule sita za Mbarara, Kashaka, Igara, Nyabubare, Ibanda na Bigyera. Mbinu za uandishi wa insha, usaili pamoja na ushuhudiaji zilitumiwa kukusanya data. Watoataarifa walikuwa wajifunzaji wa Kiswahili wa kidato cha pili hadi sita pamoja na walimu wanaofundisha Kiswahili katika shule hizo. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Usasanyuzi Dosari iliyoasisiwa na Corder, mwaka 1967. Matokeo ya uchanganuzi wa data yalibainisha kuwa wajifunzaji wa Kiswahili katika shule za upili nchini Uganda hufanya dosari mbalimbali za kimofosintaksia. Dosari hizo ni pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya vipatanishi vya kisarufi, matumizi yasiyo sahihi ya viambishi, vielezi, virejeshi, vivumishi, kuchanganya njeo, utohozi usiofaa pamoja na kutokukanusha kwa usahihi. Mwandishi anatarajia kuwa, makala haya yatasaidia walimu kubaini kwamba vipengele vya kimofosintaksia kama upatanisho wa kisarufi katika njeo, urejeshaji na ukanushi, miongoni mwa vingine, huwatatiza sana wajifunzaji na kuwasababishia kufanya dosari, hivyo, ni sharti wavimakinikie sana katika ufundishaji. Hii itawasaidia wajifunzaji kuweza kuvimudu vizuri na kuwawezesha kujifunza Kiswahili kwa fasaha.

DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na44t1.5

Downloads

Download data is not yet available.

Downloads

Published

2025-06-30

Issue

Section

Articles