Uambikaji wa Viambishi Ngeli katika Nomino Sahili Zinazorejelea Ndugu na Maana yake katika Sarufi ya Kiswahili
Abstract
Nomino sahili ni maneno ambayo kimofolojia yameundwa na mofu huru moja. Pia, kisematiki, maneno haya yana maana zake katika kamusi. Licha ya kuwa na sifa hizi, uambikaji wa viambishi ngeli {m-/mu-, ji-, ma-, ki-, ka-, tu, na u-} katika nomino hizi unaathiri sifa tajwa. Makala haya yanafafanua athari za kimofolojia na za kisemantiki za uambikaji wa viambishi ngeli katika nomino hizi na maana ya athari hizo katika ufafanuzi wa sarufi ya Kiswahili. Data zilizotumika zilipatikana kwa njia ya ushuhudiaji shiriki, hojaji na usaili. Data hizo zilifafanuliwa kwa kutumia Nadharia ya Matumizi iliyoasisiwa na Lodwig Wittgenstein (1953). Kutokana na data hizo, makala yanaonesha kwamba uambikaji wa viambishi ngeli kwenye nomino hizi husababisha athari za kimofolojia kama vile kuongeza idadi ya mofu kutoka moja kuwa mbili na kubadili aina ya nomino kimuundo. Vilevile, uambikaji huo huathiri maana ya nomino hizo kisarufi na kileksika kwa kuzingatia matumizi yake. Iwapo nomino hizi zitaendelea kupata mashiko na kisha kusanifiwa, athari tajwa zinadokeza mahitaji ya kuboresha uainishaji wa ngeli za nomino, uandikaji wa taarifa za vidahizo katika kamusi na ufafanuzi wa upanuzi na mabadiliko ya maana katika sarufi ya Kiswahili. Hivyo, imehitimishwa kwamba athari za kimofolojia na kisemantiki zinazotokana na uambikaji wa viambishi ngeli katika nomino sahili zinadhihirisha mabadiliko ya lugha na kwamba mabadiliko haya yanapaswa kuzingatiwa katika ufafanuzi wa sarufi ya Kiswahili. Kutokana na matokeo haya, imependekezwa kwamba zifanyike tafiti kuhusu uambikaji wa viambishi ngeli katika nomino sahili za makundi mengine ya nomino katika lugha ya Kiswahili.