Ruwaza za Mofimu za Ukanushi katika Vitenzi vya Kianzwani, Kimwali na Kiswahili

Authors

  • Sauda Uba Juma Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Abstract

Makala haya yanalinganisha mofimu za ukanushi baina ya lugha za Komoro na Kiswahili. Vipengele vinavyohusika katika uchunguzi huo ni mfanano na tofauti za ruwaza za mofimu za ukanushi katika vitenzi vya Kianzwani, Kimwali na Kiswahili. Suala kuu ambalo limetusukuma katika uchunguzi huu linatokana na ukweli kwamba, kuna kutofautiana kwingi kwa mitazamo ya baadhi ya wanazuoni kuhusu uhusiano wa lugha za Komoro na Kiswahili. Wapo wanazuoni wanaozichukulia lugha za Komoro kwamba zina mnasaba na Kiswahili. Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wanadai kwamba lugha hizo hazina uhusiano wowote na Kiswahili. Hivyo, utafiti huu umechunguza ruwaza za mofimu za ukanushi katika vitenzi vya Kianzwani, Kimwali na kuzilinganisha na Kiswahili ili kubaini namna zinavyofanana na kutofautiana. Kwa hakika, kuna vipengele vingine mbalimbali vya kiisimu ambavyo vingeweza kuchunguzwa katika lugha hizo. Hii haina maana kwamba aina hii ya mofimu ni muhimu zaidi kuliko aina zingine. Makala haya ni sehemu ndogo na mahususi ya utafiti wa kiisimu. Data za utafiti uliozaa makala haya zimekusanywa kupitia usomaji wa nyaraka pamoja na usaili. Uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Ulinganishaji wa Mofimu. Matokeo ya uchunguzi yameonesha kwamba Kianzwani, Kimwali na Kiswahili ni lugha zenye mnasaba mmoja na hivyo zinatokana na lugha yenye asili moja. Hii ni kwa sababu ruwaza za mofimu za ukanushi katika lugha hizo zinalingana ingawa baadhi zinatofautiana kidogo na Kiswahili. Hata hivyo, tofauti hizo ni ndogondogo ambazo zimetokana na umbali wa kijiografia uliopo baina ya wazungumzaji wa lugha hizo na wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili.

DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na44t1.8

 

 

Downloads

Download data is not yet available.

Downloads

Published

2025-06-30

Issue

Section

Articles