Mchakato wa Kutathmini Makala
Makala ya MULIKA yatatathminiwa na wasomaji wasiopungua wawili ambao watafanya kazi hiyo bila kufahamu taarifa za mwandishi. Waandishi wanatakiwa kuepuka kuonesha utambulisho wowote unaowahusu ndani ya makala ili kuwawezesha wanaoyatathmini kufanya kazi yao kwa haki. Sifa mojawapo ya watu watakaotathmini makala ni weledi katika uwanja unaofanyiwa tathmini. Mbali na kutumwa kwa watu wa kutathmini, makala yatapitiwa pia na wahariri wa jarida ili kuhakikisha kwamba yametimiza mahitaji ya jarida kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.
Miongoni mwa vipengele vitakavyozingatiwa wakati wa kutathmini makala ni walengwa wa makala, lengo la makala, mapitio ya maandiko, nadharia, mpangilio na uwasilishaji, ufafanuzi wa maudhui, uasili na uzingatiaji wa maadili, matumizi ya michoro na picha, uandishi wa matini na marejeleo.
Endapo maudhui ya makala yatakidhi mawanda na sera za jarida, makala yatatumwa kwa watathmini wawili ambao hawajulikani kwa mwandishi, kuwaomba kukubali kuyatathmini makala. Watathmini watatathmini miswada wakilenga kuangalia ubora wake katika maudhui, uwazi wa uwasilishaji, uasili, mchango wake kitaaluma na uzito wake kimaudhui na kiutafiti. Watathmini watapatiwa mwongozo utakaowaongoza wakati wa kutathmini makala. Baada ya kupata maoni ya watathmni, wahariri watapitia maoni hayo kabla ya kuyatuma kwa waandishi wa makala ili kuhakikisha kwamba maoni yaliyotolewa yanaendana na mwongozo uliotolewa. Baada ya maoni hayo kupitiwa na wahariri kujiridhisha kwamba yanaendana na mwongozo wa jarida, yatatumwa kwa waandishi wa makala ili waweze kuyafanyia kazi kisha kurejesha mswada uliozingatia maoni yaliyotolewa na watathmini wa makala. Wakati wa kurejesha makala baada ya kufanyia kazi maoni, mwandishi wa makala atapaswa kuandaa jedwali linaloonesha maoni aliyopewa na namna alivyoyafanyia kazi.
Kutokuzingatia mwongozo wakati wa kuandaa makala kunaweza kuwa sababu ya makala kutopewa nafasi katika hatua za awali za tathmini. Aidha, kutokuzingatia makataa ya kufanya marekebisho kwa waandishi wa makala kunaweza kuwa sababu ya makala hayo kutokuzingatiwa katika toleo husika.
Waandishi ambao makala yao yatakubaliwa mbali na kuandikiwa barua kujuzwa hatua ya kukubaliwa kwa makala hayo, watatumiwa nakala tepe ya makala yao pamoja na kurasa za awali zinazoonesha taarifa mbalimbali za jarida kwa marejeleo.
Jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba maoni yaliyomo kwenye makala yaliyochapishwa katika jarida hili ni ya waandishi wa makala na si lazima yakubaliane na yale ya Wahariri au Kamati ya Uhariri ya Jarida la Mulika na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kwa ujumla wake.