Taarifa kwa Waandishi

Utumaji: Muswada unaweza kuandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza na nakala-tepe kutumwa kwa baruapepe. Ukurasa wa kwanza wa makala unatakiwa kuwa na kichwa cha makala, jina la mwandishi, chuo au taasisi anayotoka, anwani ya posta, namba ya simu pamoja na baruapepe. Taarifa hizi ziandikwe juu kwenye ukurasa wa kwanza. Makala iwe imechapwa kwa kutumia programu ya Word, kukiwa na nafasi 1.5 kati ya mstari na mstari, na kukiwa na pambizo pana pande zote. Ikisiri yenye maneno kati ya 150 hadi 250 iwekwe mwanzoni mara tu baada ya taarifa za mwandishi. Makala iwe na idadi ya maneno kati ya 4000-7500 na mapitio ya vitabu maneno 800-1200. Makala itumwe kwa kioo1995@udsm.ac.tz au kioo.udsm@gmail.com

 

Tathmini ya Makala: Makala zote zitatathminiwa walau na wasomaji wawili bila kuonesha mwandishi ni nani. Waandishi wanatakiwa kuepuka utambulisho wowote unaowahusu ili wanaoitathmini wasimfahamu mwandishi.

 

Urejeleaji na Marejeleo: Urejeleaji wa andiko ndani ya matini ufanyike kwa kuanza na jina la ukoo la mwandishi na kufuatiwa na mwaka wa uchapishaji. Ikiwa ni nukuu ya moja kwa moja (u)kurasa zioneshwe, mfano Mulokozi (1996:34). Marejeleo yote yaliyotajwa ndani ya matini yaorodheshwe mwishoni mwa makala kwa mpangilio wa kialfabeti. Majina ya vitabu na majarida yaandikwe kwa italiki, anwani za tasnifu/tazmili ziandikwe bila italiki wala kuweka alama za kufunga na kufungua semi, na majina ya makala yawekwe ndani ya alama za kufunga na kufungua semi kama inavyoonekana katika mifano ifuatayo:

 

Bwenge, C. (2009). “Language Choice in Dar es Salaam’s Billboards.” Katika F.

Mc Laughlin (Ed.), The Languages of Urban Africa. London: Continuum. Kur. 152–177.

Kezilahabi, E. (2008). Dhifa. Nairobi: Vide ~Muwa Publishers Limited.

Mosha, D. (2019). Ulinganishi wa Majukumu ya Wahusika Kijinsia katika Nyimbo za Watoto na Uhalisia wake katika Malezi ya Watoto Nchini Tanzania. Tasnifu ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Petzell, M. (2012). “The Linguistic Situation in Tanzania.” Moderna Språk. 1:134-144.

Tanchini au Tanmwisho: Tanchini zitumiwe kwa uwekevu; zisiwe nyingi. Tanmwisho zichapwe kabla ya ukurasa wa marejeleo, zikiwa zimeorodheshwa kwa mfuatano wa namba.

 

Mifano na Vielelezo ndani ya Makala: Mifano yote, iwe ya isimu au fasihi, majedwali, michoro, ramani na picha vipangwe kwa unadhifu kwenye ukurasa husika na vifafanuliwe kadiri inavyobidi. Mahali pa kuweka majedwali, michoro au ramani paoneshwe kwa uwazi. Majedwali au michoro isiyokaa vizuri kwenye ukurasa haitachapwa.

 

Udanganyifu wa Kitaaluma: Kunakili maneno, mawazo, michoro, n.k., kutoka vyanzo vingine bila kuonesha utambuzi wa vyanzo husika kutafasiriwa kuwa ni udanganyifu wa kitaaluma na hivyo muswada hautakubaliwa.

 

Idhini ya Kuchapisha: Ikiwa muswada utakubaliwa, shurti mwandishi atoe idhini ya maandishi kuthibitisha kwamba kazi yake haijakusanywa wala kuchapishwa mahali pengine.